Dk. Bilal kuzindua mbio za Mwenge
Tuesday, 04 October 2011 19:35 newsroom
MAKAMU wa Rais, Dk. Mohammed Gharib Bilal, anatarajiwa kuwa mgeni rasmi katika uzinduzi wa mbio za Mwenge wa Uhuru, utakaofanyika Oktoba 14, mwaka huu, Butiama, mkoani Mara. Uzinduzi huo utafanyika pamoja na kumbukumbu ya kifo cha hayati Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere.
Akizungumza na waandishi wa habari jana, katika ukumbi wa Idara ya Habari (MAELEZO), Dar es Salaam, Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo, Dk. Emmanuel Nchimbi, alisema mbio za Mwenge wa Uhuru, zitahitimishwa Desemba 9, mwaka huu, ambayo itakuwa kilele cha miaka 50 ya Uhuru wa Tanganyika. Dk. Nchimbi alisema mbio hizo ni sehemu ya maadhimisho ya miaka 50 ya uhuru, ambapo kwa mwaka huu, Mwenge wa Uhuru utakimbizwa katika makao makuu ya mikoa pekee.
Alisema pia atazindua wiki ya maonyesho ya wizara hiyo yatakayofanyika kijijini Butiama, kuanzia Oktoba 7 hadi 14, mwaka huu.
Waziri alisema lengo la maonyesho hayo ni kuwaeleza wananchi mafanikio yaliyopatikana katika sekta zinazosimamiwa na wizara hiyo tangu uhuru hadi sasa. Dk. Nchimbi alisema vijana watashiriki shughuli za kujitolea za kijamii na machapisho ya mafanikio ya serikali na matukio ya kitaifa yataonyeshwa ili wananchi wapate uelewa mpana kuhusu historia ya nchi.
Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Mara, John Tupa, alisema maandalizi ya mbio za Mwenge wa Uhuru yamekamilika na ulinzi na usalama umeimarishwa.
Mwenge kuanza mbio mkoani Singida leo
MWENGE wa Uhuru unatarajiwa kuanza mbio zake kwa siku mbili mkoani hapa kuanzia leo. Taarifa iliyotolewa jana kwa vyombo vya habari na Mkuu wa Mkoa, Dk. Parseko Kone, ilisema Mwenge huo utaanzia katika wilaya ya Manyoni, na kwamba miradi 18 ya zaidi ya sh. milioni 400 inatarajiwa kuzinduliwa. Taarifa hiyo ilisema mbio hizo ambazo mwaka huu ni za kipekee, tofauti na ukimbizaji uliozoeleka, zinatokana na mwaka 2011, Tanzania Bara kutimiza miaka 50 ya Uhuru.
Ilisema kupitia mwenge huo, wananchi watapata fursa ya kuungana na Watanzania wengine kuwaenzi waasisi wa Taifa kwa kutunza mambo mazuri waliyoyaacha. Dk. Kone alifafanua kwamba baada ya mwenge huo kupokelewa mpakani mwa Singida na Dodoma katika kijiji cha Lusilile wilayani Manyoni, viongozi wa mkoa wa Dodoma wataukabidhi kwa viongozi wa mkoa wa Singida. Hata hivyo, alisema baada ya mapokezi hayo, mbio hizo zitaanza rasmi wilayani Manyoni, na kwamba mchana utaingia wilaya ya Singida Vijijini ambapo utamalizia mbio zake.
Katika siku hiyo ya kwanza, licha ya kuzindua miradi mbalimbali ta maendeleo, pia wakimbiza mwenge watakagua na kuweka mawe ya msingi kwenye miradi ya wananchi iliyopo katika manispaa ya Singida. Katika siku yake ya pili, Kone alisema mwenge huo utakimbizwa katika wilaya ya Iramba ambako pia miradi mbalimbali ya wananchi itakaguliwa, kuzinduliwa na kuwekwa mawe ya msingi.



No comments:
Post a Comment